Breaking News

Marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo yapita




BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 3 wa mwaka 2016, pamoja na marekebisho ya sheria tisa, ikiwemo ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB).

Katika marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, imependekezwa mwanafunzi aliyekopa alipe mkopo wake miaka miwili baada ya kumaliza au kusitisha masomo, badala ya ilivyo sasa kwamba analipa mwaka mmoja baada ya kumaliza au kusitisha masomo.

Muswada huo uliwasilishwa bungeni juzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, kwa kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu.

Baada ya mjadala na kupitia Ibara baada ya Ibara Bunge lilipokaa kama Kamati, ulipitishwa.

Mapendekezo ya marekebisho ya muda wa kulipa mkopo yalitolewa bungeni na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) yakilenga Ibara ya 18 na yaliungwa mkono na wabunge wengi wa upinzani pamoja na baadhi ya wabunge wa CCM na Serikali iliyakubadili baada ya mjadala mrefu.

Wabunge waliounga mkono hoja ya Waitara ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACTWazalendo), Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema), Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) na Mbunge wa Mbulu Vijijini, Fratei Massay (CCM).

Akichangia hoja, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema Serikali imeridhia kurekebisha kipengele hicho cha kulipa mkopo kwa aliyejiajiri au kuajiriwa na sasa mnufaika ataanza kulipa deni lake baada ya miaka miwili anapomaliza au kusitisha masomo.

Hata hivyo, sheria imeelekeza mwenye uwezo wa kulipa kabla ya muda huo, kufanya hivyo ili mikopo hiyo itolewe kwa wahitaji wengine. Awali ilikuwa mhusika analipa deni baada ya kumaliza masomo, ikarekebishwa kuwa mwaka mmoja.

Baadhi ya wabunge walipendekeza iwe miaka miwili baada ya kuajiriwa lakini Serikali ilichukua hoja ya Waitara na kuweka miaka hiyo miwili baada ya masomo.

Eneo jingine la sheria hiyo lililorekebishwa ni idadi ya wajumbe wa HELSB. Awali ilipendekezwa saba kutoka 15 lakini juzi Serikali ilirekebisha Ibara ya 17 (5) inayoweka masharti kuhusu wajumbe hao wa bodi na kufikia wajumbe tisa wanaozingatia jinsia na Muungano.

Kuhusu kiasi cha makato, kimebaki Sh 120,000 kwa mwezi au asilimia 10 ya mapato kwa aliyejiajiri badala ya Sh 120,000 au asilimia 15 ya mapato yake.

Hata hivyo kwa mtumishi aliyeajiriwa hakuna marekebisho bali atakatwa asilimia 15 ya mshahara wake na mwajiri wake.

Faini kwa mwajiri atakayeshindwa kuifahamisha Bodi kuwa mwajiriwa ni mnufaika wa mikopo ndani ya siku 28 baada ya kumwajiri mtumishi mwenye mkopo, imekuwa Sh milioni moja bila kifungo. Awali ilikuwa faini ya Sh milioni tatu au kifungo cha miezi sita jela.

No comments