Maandamano dhidi ya Trump usiku wa pili Marekani
Maelfu ya watu waliandamana usiku wa pili nchini Marekani kupinga ushindi wa mgombea wa chama cha Republican Donald Trump, ingawa hawakuwa wengi kama usiku wa kwanza.
Waandamanaji sana wamekuwa vijana ambao wanasema uongozi wa Trump utazua migawanyiko kwa misingi ya rangi na jinsia.
Hata hivyo, polisi eneo la Portland wamesema wamekabiliana na wezi na waporaji pamoja na watu wengine waliokuwa wanawashambulia wengine.
Akijibu maandamano hayo, Bw Trump ameandika kwenye Twitter kwamba "si ya haki".
Awali, alikutana na Rais Barack Obama ikulu ya White House na kumweleza kama mtu mzuri.
Hata hivyo, mwandishi wa BBC anasema licha yao kusema mkutano huo ulikuwa wa kufana, Bw Trump bado anaonekana kuwa tayari kubatilisha mambo mengi aliyoyafanya Obama alipokuwa madarakani. Miongoni mwa hayo ni Obamacare, sheria ya bima ya taifa iliyowawezesha Wamarekani wengi zaidi kuliko awali kupata bima ya matibabu.
Waandamanaji walikusanyika katika miji mbalimbal Marekani Alhamisi jioni.
Polisi mjini Portland, Oregon, walisema maandamano hayo yanafaa kuchukuliwa kama ghasia. Walisema madirisha ya maduka yalivunjwa, na baadhi ya waandamanaji walibeba magongo na mawe.
Hakukuwa na ripoti za kuzuka kwa fujo katika maandamano mengine, ingawa waandamanaji Minneapolis walifunga barabara kuu njia zote mbili kwa muda.
Mjini Philadelphia umati wa watu ulikusanyika nje ya ukumbi wa baraza la jiji na kuimba "Not Our President" (Si Rais Wetu), "Trans Against Trump" (Trans Dhidi ya Trump) na "Make America Safe For All" (Ifanye Marekani iwe Salama kwa Wote).
Mjini Baltimore, polisi walisema watu 600 waliandamana kwa amani katika barabara za mji, na kuzuia magari kupita.
Akiandika kwenye Twitter, Bw Trump aliwaeleza watu hao kama "waandamanaji wataalamu" na kusema kwamba "wamechochewa na vyombo vya habari".
Joto kimataifa
Hayo yakijiri, rais wa Mexico ameelezea matumaini kwamba taifa lake litakuwa na uhusiano mwema na Marekani chini ya Trump, licha ya kwamba amekuwa akitoa matamshi dhidi ya watu wa Mexico wakati wa kampeni.
Enrique Pena Nieto alisema yeye na Trump wamekubaliana kukutana, ikiwezekana kipindi hiki cha mpito, kabla ya Rais Trump kuapishwa Januari.
No comments