Breaking News

Mifugo kuhakikiwa nchi nzima


WAKUU wa wilaya nchini wameagizwa kuhakiki idadi ya mifugo waliyonayo kwenye wilaya zao hadi ifikapo Aprili, mwakani.

Maagizo hayo yaliyotolewa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipokuwa akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Waso wilayani hapa.

Pia ameitoa siku 30 kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuhakiki mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti unaopakana na vijiji vya tarafa ya Loliondo.

Alisema serikali imetoa agizo hilo kwa wakuu wa wilaya zote nchini ili iweze kujua idadi ya mifugo ambayo nchi inayo kwa kila wilaya na kupanga jinsi ya kuchanja mifugo ili isikumbwe na magonjwa mbalimbali.

Alisema hivi sasa mifugo inasumbua, mingine inaingia kwenye hifadhi mbalimbali huku mingine ikiibua migogoro kati ya wakulima na wafugaji, hivyo hivi sasa serikali inataka kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji.

“Wakuu wote wa wilaya hakikisheni hadi Aprili mwakani muwe mmekamilisha uhakiki wa mifugo na nyie Tanapa mpime eneo la mpaka wa Serengeti na vijiji vya Loliondo,” alisema.

Waziri Mkuu alisema mifugo hiyo ikihakikiwa itasaidia halmashauri nchini kuhudumia mifugo kwani hivi sasa wafugaji hawaoni umuhimu wa kuchanja mifugo yao.

Naye Mbunge wa Ngorongoro ambaye ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha alimshukuru Majaliwa kufika katika jimbo hilo na kujionea kero kubwa ya ardhi ambayo inawasumbua wananchi.

Alisema mgogoro wa pori tengefu la Loliondo umesababisha yeye kama mbunge kuchafuliwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari.

No comments