Breaking News

Ujumbe wa marais wa Afrika Magharibi waondoka Gambia mikono mitupu



Ujumbe wa marais wa Afrika Magharibi waliozuru nchini Gambia kumshawishi rais Yahya Jammeh kukubali kuondoka madarakani, wameondoka jijini Banjul bila ya kupata suluhu yoyote.

Viongozi wa nchi wa Nigeria, Ghana, Siere Leone wakiongozwa na rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, amesema mazungumzo yalikwenda vizuri lakini hakuna mwafaka wowote uliofikiwa.

“Tulikuja kuwasaidia watu wa Gambia. Sio jambo ambalo tunaweza kulifanya kwa siku moja.Tutaendelea kulishughulikia,” alisema Ellen Johnson Sirleaf.

Naye rais wa Nigeria, aliwaambia wanahabari kuwa rais Jammeh aliwapokea vizuri  na alionekana kuwasikiliza lakini mwafaka haukupatikana.

Wakati ujumbe huo ukikutana na rais Jammeh, wanajeshi walikwenda katika makao makuu ya Tume ya Uchaguzi na kuwaambia wafanyikazi kurudi nyumbani, hali ambayo imezua hali ya wasiwasi.

Mbali na hilo, chama cha rais Jammeh kimekwenda Mahakamani kulalamikia matokeo yalimpa ushindi Adama Barrow, ambaye amemtaka Jammeh kuondoka madarakani haraka iwezekanavyo.

Mzozo wa kisiasa nchini Gambia umekuja baada ya rais Jammeh kubadilisha msimamo wake na kukataa kuyatambua matokeo baada ya hapo awali kutangaza kuwa alikuwa amekubali kushindwa baada ya kuliongoza taifa hilo kwa miaka 22.

No comments