Gondwe acharuka Handeni
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ametoa mwezi mmoja kwa wakulima na wafugaji walioingia wilayani humo bila kufuata utaratibu wa kisheria kuondoka.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Kwamagome na Kijiji cha Kitumbi, Gondwe alisema amebaini uwapo wa migogoro isiyo ya lazima iliyosababishwa na watendaji wa vijiji na mitaa kuuza ardhi bila kufuata utaratibu wa kisheria.Kutokana na hilo, aliamuru wakulima na wafugaji wavamizi kuondoka wilayani humo.
Alisema mkulima au mfugaji anayetaka kufanya shughuli zakeHandeni lazima apate kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya na mkurugenzi, kukubali idadi ya mifugo atakayokuwa nayo na akae eneo alilopangiwa na kinyume na hilo atakuwa amevunja utaratibu.
“Hadi Desemba 20, wale wote ambao wamevamia kwenye maeneo ya hifadhi, mkulima aliye eneo la malisho, mfugaji aliyeingiza mifugo eneo la kilimo na wale ambao wameingia kwa njia za panya wote muondoke, baada ya hapo hamtaniona ila nitatuma jamaa zangu (polisi) waje kufanya kazi na sitaki lawama,” alisema Gondwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Makufwe alisema ofisi yake haitalipa fidia za kizembe kwa watendaji waliokiuka utaratibu wa kutoa ardhi.
Diwani wa Kwamagome, Mussa Mkombati alisema yapo maeneo kwa ajili ya kilimo ila wamepewa wafugaji na baadhi ya watendaji, huku yale ya wafugaji kuna wakulima wameuziwa.
Mkulima Gamalieli Kimaro, anayetakiwa kuondoka eneo la Mkuzi ambako ana shamba lenye ekari 30 alidai aliuziwa kihalali na Serikali ya kijiji.
ila hadi sasa serikali ya wilaya imedai eneo hilo ni kwaajili ya wafugaji na anatakiwa kuondoka huku akiwa tayari ameshasafishwa shamba hilo kwa gharama zaidi ya 150 milioni.
Hamisi Kidainye nae ni mfugaji katika eneo la kitumbi alidai kuwa tatizo lililopo kuna baadhi ya viongozi wa kata na vijiji wanachukua ffedha kutoka kwa wenzao wasio waaminifu na kuwapa maeneo hivyo kusababisha kutokea ugomvi mara kwa mara huku wao wakihamishwa maeneo mengine kikazi.

No comments