Breaking News

Jela sasa kuwahusu madereva wasio na leseni



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa ameamuru kukamatwa na kupelekwa gerezani madereva wa vyombo vya usafiri wasiokuwa na leseni.
Akizungumza na wananchi kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mkendo mjini Musoma wakati wa Uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, Mlingwa alilitaka Jeshi la Polisi na hasa Kitengo cha Usalama Barabarani kusimamia ipasavyo sheria ili kuokoa maisha ya watu kutokana na ajali zinazosababishwa na madereva baadhi wakiwa hawana leseni.
Kuhusu madereva wa pikipiki alisema: “Wengi wenu mnahudhuria mafunzo na kupewa vyeti lakini hamjui alama za barabarani. Ili kupata leseni naamini ni lazima dereva apewe mtihani.”
Alizitaka halmashauri zote mkoani Mara kushirikiana na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kutengeneza barabara zenye kiwango, zisizo na mabonde ambazo ni chanzo kikuu cha ajali.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Mara, Michael Deleli alisema ajali nyingi husababishwa na ulevi na utumiaji wa dawa za kulevya.
Alisema takwimu zinaonyesha ajali za barabarani mwaka 2013 zilikuwa 160 na watu 57 walipoteza maisha; 2014 zilikuwa 154 na vifo vilikuwa 108; 2015 ajali zilikuwa 137, zilizosababisha majeruhi 133 na vifo 77 na kuanzia Januari hadi Oktoba, ajali zilizotokea ni 91 zilizosababisha majeruhi 108 na vifo 84.
Deleli aliomba viongozi ngazi za kata na mitaa kusaidia kutoa elimu ya usalama barabarani kwenye mikutano na kuzungumza na wananchi ili kuwaelimisha umuhimu wa alama za barabarani.

No comments