Breaking News

Kesi ya ubadhirifu wa Kakobe kuanza disemba mosi



Baada ya kusuasua kwa muda huku ikiahirishwa mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali, hatimaye kesi ya madai ya ubadhirifu wa Sh14 bilioni inayomkabili Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe itaanza kuunguruma Desemba Mosi.
Tarehe hiyo ilipangwa jana na Jaji wa Mahakama Kuu, Lugano Mwandambo aliyepangwa kusikiliza kesi hiyo akiwa ni wa nne kupangiwa akitanguliwa na majaji Agustine Shangwa, Iman Abood na Salvatory Bongole.
Kwa mujibu wa hati ya madai walalamikaji ambao walikuwa wachungaji wa kanisa hilo Dezedelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma walifungua madai wakimtuhumu askofu huyo kukusanya fedha nyingi kutoka kwa waumini kwa madai ya kufanyia shughuli na miradi za kanisa na kuzitumia isivyo
Awali, wakati ikiwa katika hatua za awali, askofu huyo aligoma kuhudhuria vikao vya usuluhishi na jalada lilirejeshwa kwa Jaji Mfawidhi ili lipangiwe jaji wa kuisikiliza na ilipangwa isikilizwe na Jaji Imani Abood, kisha ikahamishiwa kwa Salvatory Bongole ambaye baadaye alihamishwa kabla ya kuanza kuisikiliza.
Mwenendo wa kesi hiyo umekuwa ukisuasua kutokana na kuahirishwa mara kwa mara kwa sababu mbalimbali zikiwamo majaji kujitoa, kuhamishwa na pingamizi za awali.
Baada ya kupangiwa kesi hiyo, Jaji Mwandambo amepanga kuanza usikilizwaji kwa kupokea ushahidi wa madai dhidi ya Askofu Kakobe kutoka kwa walalamikaji. Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2011 imeshaingizwa kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) wa Mahakama ambao unalenga kusikiliza na kuamua mashauri yote ambayo yamechukua muda mrefu bila kumalizika.
Hata hivyo, mmoja wa walalamikaji, Kaduma alijitoa baada ya kupata ajali na kufanyiwa upasuaji wa kichwa, lakini msimamizi wa kanisa hilo wilayani Liwale, Mkoa wa Lindi, Mchungaji Ignas Innocent ameiomba Mahakama hiyo aunganishwe na walalamikaji waliosalia.
Pamoja na tuhuma za ubadhirifu wa fedha hizo wanazodai kuwa ni mali ya kanisa, pia wanamtuhumu Kakobe kwa ukiukwaji wa Katiba.
Kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa walalamikaji kumefikiwa baada ya usuluhishi kushindikana kutokana na Kakobe kugoma kufika mahakamani.

CHANZO:MWANANCHI

No comments