Breaking News

Mbunge mwingine Chadema polisi







Waitara alikamatwa eneo la Uvikiuta alipokuwa akifuatilia mgogoro wa muda mrefu wa ardhi na kupelekwa kwenye Kituo cha Polisi Chang'ombe, Temeke jijini.
Akizungumza kwa simu jana, Waitara alidai hakuzuia jeshi hilo kutekeleza majukumu yake isipokuwa alihoji sababu za nyumba za wananchi wa Mtaa wa Uvikiuta uliopo Kata ya Ukonga kuvunjwa pasi na taarifa, na kampuni moja ya udalali chini ya jeshi hilo.
Alisema jana majira ya saa mbili asubuhi alipata taarifa za wananchi wake kuvamiwa na watu wanaojita kampuni ya madalali ambao walifika katika eneo lao na kuanza kuvunja nyumba na alipoamua kuhoji sababu za zoezi hilo kufanywa bila taarifa, alikamtwa na kupelekwa polisi kwa madai kwamba amezuia jeshi kutekeleza majukumu yao.
“Mimi sijazuia jeshi kufanya kazi yake, nilikuwa nahoji tu kwa nini iweje ghafla hivyo na ninavyofahamu mgogoro huo ulikuwa wa siku nyingi na kesi yake bado iko mahakamani," alisema Waitara. "Sasa kwa nini waje kuvunja wakati kesi inaendelea na hata hivyo wananchi hawajapewa taarifa?”
Alisema kuwa jana mchana alipewa fomu ya kuandika maelezo yake, lakini akaomba asiandike chochote mpaka awasiliane na Mwanasheria wake.
“Tangu saa nne asubuhi nilikuwa nahojiwa polisi hadi saa 12 jioni ndiyo nimetolewa. Wanadai nimezuia polisi kutekeleza majukumu yao, wamekubali kuniachia kwa dhamana lakini wameniambia niende kesho saa mbili asubuhi kwa RCO," alisema Waitara jana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Andrew Satta alitafutwa na Nipashe kuzungumzia suala hilo lakini simu yake ilikuwa ikipokewa na msaidizi wake aliyekuwa akidai alikuwa katika majukumu mengine hivyo atafutwe baadaye.
Hata alipotafutwa baadaye, hakupokea simu badala yake simu ilituma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) ulioeleza kuwa Kamanda Satta alikuwa kwenye kikao.
Waitara anaungana na wabunge wengine wa Chadema wakiwamo Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Godbless Lema (Arusha Mjini) ambao wamekuwa wakikamatwa na kutakiwa kuripoti kwenye vituo vya polisi.

No comments