Breaking News

Wananchi wamtimua mwenyekiti mbele ya wabunge


Habari mpya.Lugha ya matusi, ubadhirifu wa fedha na kuingilia majukumu ya kazi ni mambo yaliyowasukuma wakazi wa Kijiji cha Malita wilayani Maswa, kumkataa mwenyekiti wao.



Uamuzi huo wameutoa kwenye mkutano mkuu wa kijiji uliohudhuriwa na wabunge wa majimbo ya Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo na Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki. Pia, diwani wa Zanzui, Jeremiah Shigala.



Mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Malita, Emanuel Kongwa alipopewa nafasi ya kujitetea amesema mkutano huo umeandaliwa kisiasa, hivyo hautambui kwa sababu wengi waliomtuhumu ni wananchi ambao wamekuwa wakimpiga vita kwa kushirikiana na diwani Shigala.



Amedai alijua kuhusu mpango wenye sura ya kisiasa wa kumwondoa madarakani ulioandaliwa na kikundi cha watu.



Wabunge, diwani na mwenyekiti huyo wote wanatokana na CCM.

Mwenyekiti wa muda wa kijiji hicho, Mussa William amesema: “Leo (juzi) ni kikao cha mwisho kuhusu malalamiko yenu dhidi ya mwenyekiti mliyoyaleta kwangu kwa muda mrefu tangu mwaka jana, mtaamua wenyewe aendelee au la.”



William ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha Mkuyuni, amesema tuhuma dhidi ya Kongwa ni ubadhirifu wa fedha za mapato ya kijiji Sh560,000 na kuingilia kazi za mtendaji wa kijiji,  wenyeviti wa vitongoji na mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Malita.



Mbunge Ndaki ameshangazwa na tuhuma nyingi na nzito zilizotolewa na wananchi dhidi ya mwenyekiti huyo na kwamba, taarifa ya uamuzi wa wananchi wataipeleka kwa mkuu wa wilaya kwa hatua zaidi.

No comments