Breaking News

Waziri mkuu awagusa TUCTA



Kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuahidi kufanyia kazi malalamiko aliyopewa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kuhusu mtindo wa baadhi ya wateule wa Rais kutumia madaraka yao vibaya, imepata uungwaji mkono.



Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) Mkoa wa Tanga, Abbas Mbelwa ametoa shukrani kwa Majaliwa na kumtaka kuisimamia kauli yake ili iweze kutekelezeka.



“Ni ukweli usiofichika kwamba wafanyakazi nchini wamekuwa wakitenda kazi zao kwa wasiwasi kutokana na baadhi ya wateule wa Rais kutoa amri zinazokwenda kinyume na taratibu za kikazi,” amesema Mbelwa.



Amesema katika kikao cha kwanza cha kamati ya utendaji ya Tughe mkoa wa Tanga tangu ilipochaguliwa wamejiwekea lengo la kuongeza wanachama kutoka 1,352 waliopo sasa hadi kufikia 2,000 ifikapo Juni mwakani.



“Lakini pia tumeweka mikakati ya ufuatiliaji wa kero zinazowahusu watumishi ikiwamo madai ya muda mrefu ya malimbikizo kuongezewa mishahara,madaraja na likizo wanayoidai serikalini,” amesema Mbelwa.



Juma Ali ambaye ni mtumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo amesema wanadai malimbikizo ya muda mrefu ya malipo ya likizo licha ya kwamba walishasainishwa fomu za kulipwa.


No comments