Breaking News

Jaji mkuu atema cheche kwa mawakili na polisi.




Emmanuel JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman, amewavaa mawakili na kuwaambia wazi kuwa baadhi yao wanatumiwa na wateja wao wenye kesi kwa ajili ya kuchelewesha kesi mahakamani, kitu ambacho ni kinyume na maadili ya kazi hiyo.

Aidha, Jaji Chande amesema pia kuwa mbali na mawakili, pia Polisi, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mahakama, nao wanachangia mrundikano wa kesi, hivyo kukwamisha masuala mbalimbali.

Amezitaka taasisi hizo, kutotumika kuchelewesha kesi, badala yake waisaidie mahakama katika mpango mkakati wake wa kupunguza mrundikano wa kesi.

Alisema hayo wakati wa hafla ya kuwaapisha mawakili wapya 285, iliyofanyika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana. Kuapishwa kwao kunafanya idadi ya mawakili nchini kufikia 6,082. Jaji Othman alisema kuwa wapo baadhi ya mawakili, wanatumiwa na wateja wao kwa ajili ya kuchelewesha kesi, kitu ambacho ni kinyume na maadili ya kazi hiyo.

“Tunawasisitiza mawakili hawa wawe sehemu yaLipumba mrundikano wa kesi ili kufikia mipango mikakati yetu ya miaka mitano kuanzia 2015 hadi 2020,” alisema Chande.

Aidha, alisema kuwa wamepokea asilimia 71 ya malalamiko kutoka kwa wananchi, ambapo asilimia 45 ya malalamiko hayo, yalionekana kuwa ya kweli kwamba wanasheria wafanya kazi zao bila kuzingatia taratibu na maadili yaliyowekwa.

Alisema wateja wamekuwa wakilalamika kwamba wanapotoa siri zao kwa mawakili, zinatolewa nje na kuwa wengi wao, hawawatetei wateja kama inavyotakiwa. Hata hivyo, alisema kuwa wapo mawakili ambao leseni zao za kufanya kazi zinapoisha, hawachukui mpya, hivyo kushindwa kuendelea na kazi hiyo.

Aliongeza kuwa ni vyema mawakili hao, wazingatie sheria na maadili ya kazi hiyo na kuendelea kuongeza ujuzi wa sheria kwa kuwa elimu waliyoipata haitoshi. Vile vile, aliwaagiza mawakili hao kufanya kazi mikoani na sio kurundikana mijini, kwa kuwa ipo baadhi ya mikoa yenye mawakili wasiozidi 10.

“Mawakili wafike na mikoani ikiwemo Lindi, Tabora, Lindi ambayo wananchi wanahitaji huduma hiyo, lakini hakuna mawakili wa kuwasaidia,” alisisitiza Chande.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Ferdinand Wambari alisisitiza kuwa watanzania wanataka kuona ushiriki wa dhati katika masuala ya haki, kwa kuwa waaminifu na wanaowawakilisha vyema kwa mujibu wa sheria.

Wambari alisema hawategemei kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi, kwa kuwa wanaamini watafanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia matakwa ya sheria.

No comments