Mwakyembe agoma IJA kuwa chuo kikuu
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema hayupo tayari kuona Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kinapandishwa hadhi na kuwa chuo kikuu, kwa sababu jukumu lake la kuwanoa vijana ngazi za chini na kati kwenye fani ya sheria, bado linahitajika nchini.
Badala yake, aliahidi kutoa ushirikiano ili kitekeleza majukumu yake ikiwamo kutoa msukumo wa kupelekewa kasma ya kukiendesha kwa wakati, kutekeleza dhamira ya kutoa mafunzo ya Mahakama kwa majaji, mahakimu na watendaji wanaohusika na utoaji haki.
Dk Mwakyembe alibainisha hayo wakati wa mahafali ya wahitimu wa astashahada na stashahada ya chuo hicho, yaliyofanyika mjini Lushoto. Aliahidi kushirikiana na wizara nyingine kuhakikisha watumishi wake wanaohusika kwa namna moja au nyingine katika masuala ya sheria, wanapelekwa IJA kwa ajili ya kunolewa ili kutenda majukumu yao kwa weledi zaidi.
Alisema ni muhimu ikaeleweka kwamba madhumuni ya msingi ya uanzishwaji wa IJA, ni kutoa mafunzo endelevu ya Mahakama kwa ajili ya kuwanoa na kuwapa weledi stahiki watumishi wote wa idara hiyo na wadau wa sheria wakiwamo waendesha mashtaka, mawakili wa Serikali maofisa magereza, Takukuru na Polisi.
Waziri huyo alisema anatarajia kuwasilisha kwa mara ya pili bungeni Muswaada wa Msaada wa Huduma za Sheria katika kikao kijacho cha Bunge na kwamba, utakapopitishwa utawapa ‘meno’ wahitimu wa stashahada chuoni hapo kutoa huduma za kisheria kwa wananchi.

No comments