Breaking News

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kukagua akaunti za bandari


MKAGUZI na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ametakiwa kufanya ukaguzi maalumu katika akaunti, zilizofunguliwa kwenye benki mbalimbali za muda maalumu za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), zenye thamani ya Sh bilioni 440 zilizofunguliwa na riba ndogo.

Agizo hilo limetolewa mjini hapa jana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati ilipomaliza kupitia na kujadili hesabu za mamlaka hiyo za mwaka wa fedha 2014/15.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, katika ukaguzi wa mwaka ujao, CAG anatakiwa ashirikiane na Benki Kuu ya Tanzana (BoT) na Kitengo cha Uchunguzi wa Fedha na kubainisha kiasi cha riba kilichokubaliwa na faida iliyopatikana.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly alizitaja benki zilizofunguliwa akaunti hizo na TPA kuwa ni NMB, CRDB, Standard Chartered na NBC.

Agizo hilo la kamati limetokana na michango ya wajumbe wa kamati hiyo wakati wa kujadili hesabu za TPA zilizokaguliwa na CAG na kubainika kuwepo kwa akaunti hizo, lakini zikiwa zimefunguliwa kwa riba ndogo tofauti na kiwango cha fedha hizo.

Akitoa agizo la kamati kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka, alisema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa na kutokana na riba hiyo ndogo TPA imepoteza mabilioni ya fedha, hivyo ni vyema ufanyike uchunguzi ili kubaini kwa nini benki hizo zimetoa riba hiyo ndogo kwa kiasi kikubwa cha fedha hizo.

Awali, wakati akichangia katika mjadala wa kamati hiyo, Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM) aliufananisha ufisadi wa akaunti hizo kama ule wa Kishapu wa jumla ya Sh bilioni tano ambao baada ya kusimamiwa ipasavyo fedha hizo zilipatikana.

Maige alisema endapo mtu anaweka fedha benki kupitia akaunti hiyo ya muda maalumu, benki huweka viwango vya riba kulingana na kiasi cha fedha kilichowekwa kwenye akaunti husika.

“Kwa sasa wastani wa chini viwango vya riba ni asilimia 7.5 na kiwango hicho huongezeka kutokana na kiasi cha fedha ambacho mteja anaweka kwenye akaunti,” alisema baadaye wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ufafanuzi wa suala hilo.

Alisema kwenye benki nyingi asilimia 7.5 hulipwa kama kiwango cha fedha kilichowekwa kiko chini ya Sh milioni 500, lakini kwa baadhi ya benki ikiweka zaidi ya Sh milioni 500 hadi bilioni mbili inayolipwa inapanda na kufikia asilimia tisa na ikizidi Sh bilioni mbili hupanda na kufikia zaidi ya asilimia 13.

“TPA kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2015 ilikuwa imeweka bilioni 440 kwenye fixed akaunti, kiwango hicho kinapatiwa kiwango cha riba ambacho ni zaidi ya asilimia 13,” alisema Maige.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na CAG na kwa mujibu wa ripoti yake riba iliyolipwa TPA kutokana na akaunti za fedha hizo ni Sh bilioni 17 ambayo ni sawa na kupata riba ya chini ya asilimia mbili badala ya zaidi ya asilimia 13. Kiwango halisi walichopaswa kulipwa ni bilioni 57 kwa mwaka.

“Kimsingi TPA imepoteza zaidi ya Sh bilioni 32, kwa makusudi kabisa na hii ni motive ya kifisadi, maofisa wa bandari walikuwa wanakubaliana na benki riba za chini na kiasi ambacho mamlaka ilistahili kupata wanaishia kugawana,” alidai.

Alisema kutokana na ugunduzi huo, hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya maofisa wa benki na TPA watakaobainika kufanya ubadhirifu wa fedha hizo ikiwa ni pamoja na kutakiwa kuzirejesha.

Kwa upande wa Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim Ally alishauri uchunguzi huo uihusishe na BoT kwa kuwa ndio msimamizi wa taasisi za benki nchini na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote walioshiriki kuiba fedha hizo.

Alisema kuna tatizo kubwa ndani ya mamlaka hiyo na kusisitiza umuhimu wa fedha hizo zilizopotea kutokana na tozo hiyo ndogo ya riba zirejeshwe.

Naye Aesh alisisitiza kuwa pamoja na uchunguzi wa sakata hilo, lazima benki zote zilizohusika na wizi huo wa fedha kupitia riba, nazo ziwajibishwe kwa kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kilichopotea kinarejeshwa TPA.

Alisema katika uchunguzi huo wa CAG pia ubainishe ilikuwaje hadi benki hizo na TPA zikaingia.

No comments