Breaking News

Mtanzania azishitaki Kenya, Rwanda kuhusu EPA

MKAZI wa Arusha, Costa Shirima (45) amefungua kesi katika Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki akizishitaki Kenya na Rwanda kwa kuingia mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi wa EPA, kati ya Jumuiya ya Ulaya (EU) na ya Afrika Mashariki (EAC), bila ya nchi nyingine kukubaliana na kujiridhisha, wakati wakifahamu kuwa ni kinyume cha makubaliano.
Mbali ya kuzishitaki nchi hizo, Shirima ameweka pingamizi katika mahakama hiyo kuzizuia nchi za EAC kuendelea na mchakato wa kuingia mkataba huo mpaka kesi ya msingi itakaposikilizwa katika mahakama hiyo.
Kesi hiyo ilikuwa isikilizwe jana katika mahakama hiyo mbele ya jopo la majaji watano wakiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Awali ya EAC, Jaji Monica Mgenye, lakini ilishindikana kutokana na mlalamikaji kushindwa kuwasilisha taarifa ya kuitwa mahakamani kwa wakati kwa nchi zote za EAC.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Mgenye aliahirisha kesi hiyo kwa wiki mbili hadi Desemba 8, mwaka huu na kumpa nafasi Shirima kuhakikisha anatoa taarifa ya maandishi ya kuitwa mahakamani kwa nchi zote za EAC ili zifike mahakamani hapo kujibu hoja hizo.
Kwa mujibu wa jalada la kesi hiyo Namba 8/2016, ilidai Rwanda na Kenya zimekiuka makubaliano ya awali ya Baraza la Mawaziri la EAC lililoketi jijini Dar es Salaam na viongozi wakuu wa jumuiya hiyo waliotoa muda wa miezi mitatu kutafakari kwanza kama kuna umuhimu wa jumuiya hiyo kuingia Mkataba wa EPA.
Shirima alidai kuwa kabla ya muda kufika Rwanda na Kenya zilisaini mkataba huo na kukiuka kwa makusudi makubaliano ya awali na kutaka majaji wa EAC kusitisha kazi nzima ya mchakato huo kwani nchi hizo zimekiuka makubalino mpaka kesi ya msingi itakapomalizika kusikilizwa na kutolewa maamuzi.
Mbali ya Jaji Kiongozi Mgenye, majaji wengine ni Jaji Msaidizi Kiongozi, Isaac Lenaola, Jaji Faustini Ntezilyano, Jaji Fakihi Lundu na Jaji Audace Ngiye. Mawakili wa serikali watatu waliiwakilisha Uganda, na Tanzania ilikuwa na wanasheria watano huku Kenya iliwakilishwa na wanasheria watatu.
Wanasheria wa Kenya walifika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo baada ya kupewa taarifa rasmi ya kuitwa mahakamani lakini mawakili wa serikali wa nchi za Rwanda, Burundi na Sudan Kusini hawakufika kwa kuwa hawakuwa na taarifa za kuitwa mahakamani.
Mahakama ilimweleza Shirima kuhakikisha anatoa taarifa rasmi kwa wanasheria wa serikali za nchi hizo na Desemba 8, wanapaswa kufika mahakamani hapo bila ya kukosa. Wakati kesi hiyo ikifunguliwa katika mahakama hiyo, mkataba huo hivi karibuni uliwasilishwa bungeni na serikali ili kupata ushauri wa wabunge kabla serikali haijauridhia.

No comments